Wednesday, August 13, 2014

MAITI YA MTANZANIA YAWEKWA MOCHWARI KWA MIEZI NANE(8)

Majonzi vilitawala katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Agosti 7, mwaka huu kufuatia kuwasili kwa mwili wa mwanafunzi wa kidato cha nne, Habiba Yusuph Ally (24) aliyefariki dunia kwa kubakwa nchini China miezi nane iliyopita.Tukio hilo linaweka historia ya kusikitisha kwenye familia ya mzee Yusuph Ally kwa kuwa na msiba miezi nane wakati mwili wa binti yake ukiwa mochwari nchini humo baada ya kifo chake.
mtaakwamtaa14.blogspot.com


KWA NINI MIEZI NANE?
Baba wa marehemu alisema kilichosababisha maiti ya binti yake ikae mochwari kwa muda wote huo ni utafutaji wa fedha kuwa mgumu lakini hatimaye Watanzania waishio nchini humo walifanikisha na kuuleta kwa ndege ya Shirika la Ndege la Emirates.


ALICHOKIONA BABA CHAMSHTUA
Mara baada ya mwili huo kuwasili,kilifika kipengele cha kufunuliwa ili baba mzazi amtambue marehemu ambapo zoezi hilo lilimshtua mzee huyo kufuatia kuuona uso wa mwanaye ukiwa na majeraha kibao huku tumbo likiwa limeshonwa. Ilidaiwa ulifanyiwa uchunguzi.


MWILI WAPELEKWA NYUMBANI
Baada ya hapo, mwili huo ulipekekwa nyumbani kwa mzee Yusuph kwa ajili ya kuagwa na siku iliyofuata, Agosti 8, mwaka huu ukazikwa kwenye Makaburi ya Magomeni Mikumi jijini Dar es Salaam.


HABIBA ALIVYOKUFA
Maelezo ya habari yaliyotolewa na rafiki wa karibu wa Habiba aitwaye Saada yalisema siku ya tukio, marehemu alikutana na Mnigeria mmoja ambaye walipatana kulala wote kwa usiku mzima.
Alisema kumbe Mnaigeria huyo alikuwa na wenzake wanne. Usiku walimwingilia wote kwa nguvu mpaka akapoteza maisha palepale. Ulikuwa ukatili mkubwa.


Watu hao walipogundua Habiba amefariki dunia waliuchukua mwili wake na kuutupa chini kutoka ghorofa ya tano walikokuwa wamempeleka kulala naye.
Habari zaidi zilidai kuwa madaktari waliokuwa wakiuchunguza mwili wa Habiba waligundua haukuwa na figo na moyo jambo lililozidi kuzua hofu juu ya mauaji yake.
Hata hivyo, kwa mujibu wa mzee Yusuph juzi, Wanigeria hao walikamatwa na jeshi la polisi nchini humo na kufikishwa mahakamani kwa kudaiwa kuua.


Alisema mara baada ya kifo, polisi nchini humo waliizuia maiti yake kwa muda ili kupisha upelelezi zaidi na baada ya kukamilika ndipo Watanzania walioko huko wakaanzisha mchango wa fedha kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania, China na kuusafirisha mwili wake.


MBONGO
Mtanzania anayeishi kwenye Mji wa Guangzhou nchini China (jina tunalo) ambaye alidai nguvu kubwa ilitumika kuchangishana fedha ili kuuleta Bongo mwili wa marehemu Habiba.


ATOA USHAURI
Mbongo huyo anayefanya biashara nchini humo alitoa ushauri kwa Watanzania wenye ndugu China kuwa makini nao kwa vile wengi wakifa, kama hakuna moyo wa kuchangiana huzikwa na taasisi zinazosimamia kazi hizo lakini ikibainika kuwa kuna michango inayoendelea, mwili unaweza kuwekwa mochwari hata miaka miwili.


HISTORIA YA MAREHEMU HABIBA
Marehemu Habiba aliondoka Bongo kwenda China mwaka 2010 akiwa na miaka 19 akisoma kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Kiluvya, Kinondoni, Dar kufuatia kurubuniwa na mwanamke mmoja aliyetajwa kwa jina moja la Chausiku.

Chanzo cha habari: GPL

No comments:

Post a Comment