Jakaya Mrisho Kikwete, rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania anatarajiwa kuahirisha Bunge Maalum la Katiba ili kusaka suluhu baina ya CCM na Ukawa, imethibitishwa.
Tayari kamati ya uongozi ya Bunge maalum la Katiba imetaarifiwa kuhusu suala hilo na sasa inalijadili kabla ya kumpa rais Kikwete taarifa itakayopelekea kuahirisha bunge hilo.Hii inafuatia msimamo wa UKAWA na msimamo mpya wa baadhi ya wabunge wa CCM wa bunge hilo kuanza kupanga kulisusia kama litaendelea kwa namna lilivyo.
Taarifa ambazo bado hazijathibitishwa ambazo zinatoka ikulu ya Tanzania ni kwamba kuna kikao ambacho kinatarajiwa kufanyika punde tu rais Kikwete atakaporejea kutoka nje na hii ni baada ya kuahirisha Bunge hilo maalum ili kuanza mchakato wa kusaka maridhiano katika mchakato wa katiba mpya unaoendelea. Aidha shinikizo hilo limefuatia baada ya wabunge wengi wa CCM wanaounda Bunge Maalum la Katiba kutishia kuususia mchakato wa katiba mpya unaoendelea. Pia wajumbe hao wameonya kwamba ni lazima kila kiungo kinachoshiriki kuiunda katiba hiyo kiheshimiwe na hasa tume ambayo wamedai kuwa inavunjiwa heshima na watu wasioelewa nini maana ya mchakato wa katiba.
Kutakuwapo na kikao ambacho kitawashirikisha viongozi wakuu wa serikali,viongozi wa bunge maalum lakatiba na wajumbe wa tume ambapo watautafakari upya mchakato huo na kisha kuomba maridhiano na UKAWA ili kuendelea na bunge hilo, imethibitishwa.
Aidha CCM inaelekea kubadili msimamo na sasa kuna uwezekano mkubwa wa kurudia kulijadili suala la serikali tatu ambazo hazitaathiri kwa kiasi kikubwa muundo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kama wananchi walivyopendekeza.Lakini chanzo hicho kutoka ikulu ya Tanzania kimeonya kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano bado atakuwa na madaraka makubwa ili kuzuia uwezekano wa kuvunjika kwa Muungano.
No comments:
Post a Comment